LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 17, 2018

PROF. MBARAWA AAHIDI KUKAMILIKA KWA UJENZI WA DARAJA LA MTO MARA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Gemen Engineering & Mayanga, Mhandisi Andrew Nyamtori (kulia), alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Mto Mara, linalounganisha Wilaya ya Tarime na Serengeti, Mkoani Mara.
Muonekano wa Daraja la Mto Mara lenye urefu wa Mita 94 na kuunganisha Wilaya za Tarime na Serengeti likiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake. Daraja hilo litagharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Bi. Bertha Bankwa, wakati akikagua kiwanja hicho. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), akifafanua jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (wa pili kulia) mara baada ya kukagua ujenzi wa Daraja la Mto Mara, linalounganisha Wilaya ya Tarime na Serengeti, Mkoani Mara.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia), kuhusu eneo ambalo litachukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, mkoani humo.
Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma, Bi. Bertha Bankwa, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa eneo ambalo litajengwa jengo la abiria, wakati akikagua maendeleo kiwanja hicho, Mkoani Mara.
Muonekano wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Musoma, ambacho kipo katika mpango wa upanuzina uboreshaji wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, taa pamoja na jengo la jipya la abiria.



Serikali imesema ujenzi wa daraja la mto Mara lenye urefu wa mita 94 lililopo katika barabara ya Tarime-Mugumu-Nata litakamilika mwanzoni mwa mwezi wa nne mwaka huu.

Amezungumza hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua ujenzi wa daraja hilo ambalo linaunganisha wilaya ya Tarime na Serengeti na kuwatoa hofu wananchi wa wilaya hizo kuwa endapo daraja hilo likikamilika litaondosha adha waliyokuwa wanaipata ya kuvuka hasa vipindi vya masika.

“Niwahakikishieni daraja hili litamalizika mapema mwezi wa nne pia nimemuagiza mkandarasi huyu ambaye ni mzawa kuhakikisha anazingatia viwango na wakati” amesema Prof. Mbarawa.Ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo itakuwa dira kwa wakandarasi wazawa kupewa miradi mikubwa kwani pamekuwa na changamoto kwenye utekelezaji wa miradi hususani kwa wakandarasi wazawa.

Kwa upande wake Mkandarasi wa kampuni ya M/S Gemen Engineering & Mayanga, Mhandisi Andrew Nyamtori, amesema kuwa mradi umekamilika kwa sehemu kubwa hivyo kazi zilizobakia ni kutandika vyuma juu ya daraja ili likamilike na kuanza kutumika na hivyo kuiomba Serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa kwa kuwapa miradi mingine mikubwa.

“Nikuhakikishie Mhe Waziri mradi huu utakamilika kwa viwango hivyo naomba utuamini na hata zikitokea kazi nyingine naomba tupewe kipaumbele wa kuzitekeleza kwa kuwa tunaweza”, alisisitiza Mhandisi Nyamtori.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mara Mhandisi Mlima Ngaile, amesema watahakikisha wanamsimamia vizuri mkandarasi ili aweze kutekeleza mradi huo kwa viwango vyote. 

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa, amekagua kiwanja cha ndege cha Musoma na kueleza kuwa Serikali tayari imeshatangaza zabuni ya upanuzi wa kiwanja hicho na kuwa wakati wowote zabuni zitafunguliwa ili mzabuni kuweza kupatikana.

Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Musoma aliemaliza muda wake Bi. Bertha Bankwa, amesema kuwa tayari Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA) imeshaainisha hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo kinachosubiriwa kwa sasa ni kupata mkandarasi ili upanuzi na uboreshaji uanze.

Ameongeza kuwa wameshamaliza zoezi la kupitia tathimini za fidia za mali za wananchi watakaothiriwa na upanuzi wa uwanja huo ambapo jumla ya wananchi 135 wameashafanyiwa tathimini hiyo.Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku mbili mkoani Mara ikiwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages