Tuesday, July 11, 2017

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA BORA KUHAKIKISHA HUDUMA ZA SIMU ZINAKUWA BORA MIJINI NA VIJIJINI

Mama Samia
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kusimamia na kuweka mazingira bora yatakayosaidia mamia ya wananchi nchini kuhakikisha wanapata huduma za mawasiliano ya simu kwa njia ya kisasa zaidi mijini na vijijini.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati anafungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Kampuni za Simu Duniani (GSMA MOBILE 360) Jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassana amesema anaimani kuwa wadau hao wa makampuni ya simu watajadili kwa kina namna bora ya kufikisha mawasiliano ya kisasa kwa wananchi na kuweka mipango mizuri ya kufikia wananchi wengi zaidi hasa maeneo vijijini ambayo baadhi ya maeneo hayafikiki kutokana na uduni wa miundombinu.

“Ningependa kusema kwamba Tanzania inakubali sana ushirikiano na GSMA na tunatamani kupanua ushirikiano wetu na uwezeshaji kwa Watu wetu kwa njia ya sekta ya simu ili kufikia utekelezaji wa ajenda za Maendeleo endelevu ya Umoja wa Afrika AU na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020”.Amesisitiza Makamu wa Rais.

Ameleeza kuwa kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi kadhaa Kusini mwa Bara la Afrika ambayo inafanya vizuri kwa wananchi wake kutuma fedha kwa kutumia simu za mkononi na kusema kuwa hilo ni jambo zuri hasa kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na akaunti za benki hivyo huduma hiyo huwasaidia kwa kiasi kikubwa kwa kutuma fedha kwa urahisi.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa zaidi kwa huduma za kisasa za kimtandao ili wananchi waweze kunufaika zaidi kwa njia hiyo katika sekta za elimu,afya, kilimo, biashara na masuala ya kijinsia.

Amewahakikishia wadau hao wa makampuni ya simu kuwa Serikali ya awamu ya Tano itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarisha huduma zake kwa njia ya kisasa kwa wananchi.

Makamu wa Rais amesema kuwa Serikali ya itaendelea kujifunza kutoka nchi zingine ambazo zimefanya vizuri katika sekta ya mawasiliano ili taifa na wananchi wake liweze kunufaika ipasavyo na huduma hizo kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa amesema akizungumza katika mkutano huo ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Makampuni ya Mawasiliano ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa na ubora unaotakiwa.
Share:

KUCHAGUA LUGHA

IDADI YA WATU AMBAO HUTEMBELEA BLOGU HII

KUMBUKUMBU ZA POSTI ZOTE

JISAJILI UPATE TAARIFA KWA EMAIL

Jisajili ili upate taarifa kwa email

Google+ Followers

Powered by Blogger.