Kingunge asidhani kuwa Kikwete,
Mangula au Kinana 'watachafuka' kwa kuwatungia uongo
Na
Charles Charles
JUZI, Jumapili, mwanachama wa zamani
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale - Mwiru alinukuliwa na gazeti
moja la kila siku nchini, akidai kuwa hatua ya karibuni ya kuadhibiwa kwa
baadhi ya waliokuwa wanachama, ni mwendelezo wa makosa yaliyofanywa mwaka
2015 yakiongozwa na viongozi wakuu watatu wa chama hicho kilichopo
madarakani.
Viongozi aliodai kuwa kimsingi ndio
wanaopaswa kubeba dhamana ya usaliti ndani ya CCM ni Mwenyekiti Mstaafu wa
Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete; Makamu Mwenyekiti (Tanzania Bara), Philip Mangula
na Katibu Mkuu, Komredi Abdulrahman Kinana.
Alidai kuadhibiwa kwa viongozi
kadhaa ikiwemo kufukuzwa uanachama kati yao, kusimamishwa uongozi ama kupewa
onyo kwa makosa ya usaliti siyo jambo jipya, badala yake ni mwendelezo wa
makosa yaliyotokea wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea wa kiti cha Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho mwaka 2015.
Kingunge ambaye mwaka huo alijivua
uanachama wa CCM kwa kuzingatia Ibara ya 13(1)(f) ya Katiba ya Chama Cha
Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 iliyokuwa ikitumika hadi siku tisa
zilizopita, alidai kwamba Kikwete, Mangula na Kinana kwa pamoja, walifanikiwa
kuishawishi Kamati Kuu ya CCM kuvunja Katiba na Kanuni zake.
Kutokana na hali hiyo, mzee huyo
ambaye sasa ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
alisema Kamati Kuu ilishindwa kufanya kazi zake kama inavyoelekezwa na Katiba
na Kanuni na kujikuta imekataa kuwaona, kuwasikiliza ama kuwahoji wana CCM 38
waliokuwa wameomba uteuzi wa kugombea nafasi ile ya urais.
"Hawa waliohukumiwa,
wamehukumiwa kwa usaliti wa kuendana na mchakato wa kumpata mgombea urais
(mwaka 2015). Sasa swali linalokuja hapo ni je, nani aliyesalitiwa? Ni CCM
ndiyo imesalitiwa au kuna mgombea fulani maalum (wa urais) ndiye
amesalitiwa?" Alihoji.
Akizungumzia utaratibu, Kingunge pia
alisema kuwa Kamati ya Maadili ni kitengo kilichopo ndani ya Ofisi ya Katibu
Mkuu, hivyo haitambuliwi ndani ya Katiba ya CCM, lakini alificha ukweli kwamba
michakato yote ya chaguzi katika chama hicho huzingatia Katiba na Kanuni.
"Kwa hiyo, Kamati ya Maadili
haina majukumu ya Kikatiba ya kuwa na kauli juu ya nani awe au asiwe mgombea,
lakini inaweza kuishauri CC (akimaanisha Kamati Kuu) na NEC (ama Halmshauri Kuu
ya Taifa) na Kamati hiyo haiwezi kutoa ushauri wa kuvunja Katiba na
anayeshauriwa ndiye mwamuzi ", alisema.
Lakini wakati mzee huyo akidanganya
hivyo kutokana na chuki zake za sasa za kisiasa katika upande wa kwanza, na pia
kutokana na mahaba yake makubwa kwa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward
Lowassa aliyehama naye kutoka CCM mwaka 2015 anajua, tena kwa usahihi kuwa kuna
Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la Februari, 2010 ambazo alishiriki kuzitunga
na bado zinaendelea kutumika hadi sasa.
"Katiba ya Chama ndiyo sheria
kuu ya Chama Cha Mapinduzi inayoonyesha Organaizesheni ya Chama, Malengo na
Madhumuni ya Chama. Vilevile inaainisha Haki, Wajibu wa Mwanachama, Sifa,
Miiko, Majukumu ya Utendaji, Uongozi na Vikao vya Chama", kinasema Kifungu
Kidogo cha Nne cha Utangulizi cha Kanuni za Uongozi na Maadili kinachozungumzia
Katiba ya Chama Cha Mapinduzi na kuongeza:
"Utekelezaji wa Katiba ya CCM
umefafanuliwa pia katika Kanuni mbalimbali za Chama kama zilivyotolewa na
kusimamiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kufuata na kutii Katiba ya CCM na
Kanuni zake ni wajibu wa kila mwanachama wa CCM".
Mbali na kifungu hicho, Ibara ya
2(2)(i) inayozungumzia "Muundo wa Kamati ya Usalama na Maadili"
inasema:
"Ni dhahiri kwamba kazi za
Kamati za Usalama na Maadili zitakuwa muhimu sana katika kipindi hiki (cha
uchaguzi), na kwamba kazi hizo zitaongezeka. Lakini haitawezekana kuzisimamia
kwa ufanisi kazi zote hizi kutoka Makao Makuu; lazima usimamizi wa Maadili ufanywe
na kila ngazi ya uongozi kutoka taifa hadi tawi la CCM.
"Kwa hiyo, Kamati za Usalama na
Maadili zitaundwa katika kila ngazi, na kwa jinsi kazi zenyewe zilivyo, Kamati
hizo lazima ziwe ndogo ili kutunza siri. Kwa hiyo, Muundo wa Kamati hizo
utakuwa ufuatao:
"(i) Ngazi ya Taifa
(a) Mwenyekiti wa CCM - Mwenyekiti
(b) Makamu wawili wa Mwenyekiti
wa
CCM - Wajumbe
(c) Katibu Mkuu wa CCM -
Katibu
(d) Makamu wa Rais - Mjumbe
(e) Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Bara na
Zanzibar
- Wajumbe
(f) Wajumbe wanne wa Kamati
Kuu,
wawili
kutoka Bara na wawili kutoka
Zanzibar,
(jinsia ikizingatiwa) -
Wajumbe" (mwisho wa kunukuu).
Tukizingatia ushahidi huo, Kingunge
anakujaje na uongo kwamba Kamati ya Usalama na Maadili ni kitengo tu cha ndani
ya Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM?
Hivi kwa mfano hivi sasa maana yake
ni kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli; Makamu Mwenyekiti wa CCM
(Zanzibar), Dk. Ali Mohammed Shein; Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania
Bara), Philip Mangula au Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania , Samia Suluhu Hassan ni watumishi wa Kitengo cha Maadili ofisini kwa
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana?
Kuhusu Majukumu ya Kamati ya Usalama
na Maadili, Ibara ya 3(1) - (2) ya Kanuni za Uongozi na Maadili inasema, na
hapa ninanukuu:
"Kikao chenye jukumu la
Kikatiba la kusimamia mwenendo mzima wa nidhamu ya Chama ni Halmshauri Kuu ya
Taifa, lakini madaraka ya utekelezaji yamo mikononi mwa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa.
"Kwa hiyo, wajibu wa Kamati ya
Usalama na Maadili ya kila ngazi ya Uongozi wa Chama ni kuiwezesha Kamati Kuu
kutekeleza kwa ufanisi zaidi kazi zake za siku kwa siku za kusimamia nidhamu ya
wanachama na viongozi wa CCM ndani ya mfumo wa vyama vingi. Kamati Kuu ndiyo
itakayoamua jambo gani lifikishwe Halmashauri Kuu ya Taifa na lifikishwe (kwa)
namna gani".
Aidha, Ibara ya 3 ya Kanuni za
Uongozi na Maadili inayohusu kazi za Kamati hiyo katika kila ngazi, Kifungu
Kidogo cha (vii) kinasema ifuatavyo:
"Kwa sababu hiyo, Kamati za
Usalama na Maadili zitachambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba uongozi,
ama viongozi wanaoteuliwa katika ngazi mbalimbali za Chama, kabla vikao
vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi huo au
wateuliwe kushika nafasi zilizokusudiwa".
Je, mpaka kufikia hapo Kingunge bado
ana nyongeza gani kuhusu upotoshaji wake kuwa eti Kamati ya Usalama na Maadili
ni kitengo, tena ambacho kimo ofisini tu kwa Katibu Mkuu wa CCM?
Ni kweli kuwa kwa ushahidi huo wote
kuhusu Kanuni za Uongozi na Maadili kwa kunukuu Ibara ya 1(iv), 2(1) -
(2)(i)(a) - (f), 3(1) na (3)(vii), Kingunge bado ana swali ama uongo mwingine
kuhusu uwepo, uhalali na majukumu ya Kamati ya Usalama na Maadili?
Kuhusu madai kuwa Kikwete, Mangula
na Kinana walifanikiwa kuishawishi Kamati Kuu ya CCM kuvunja Katiba, Ibara ya
109(6) ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2012 iliyokuwa inatumika
wakati huo inasema, na hapa pia nanukuu:
"Unapofika wakati wa uchaguzi,
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itashughulikia mambo
yafuatayo", kisha Kifungu Kidogo cha (b) ndipo kinabainisha kuwa:
"Kufikiria na kutoa mapendekezo
yake kwa Halmshauri Kuu ya CCM ya Taifa juu ya majina ya wanachama wasiozidi
watano wanaoomba kugombea kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania".
Katika kutimiza jukumu lake hilo
mwaka 2015, Kamati Kuu ilipendekeza majina matano ya aliyekuwa Katibu wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayesimamia Idara ya Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Balozi Mstaafu wa Umoja
wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Amina Salum
Ali; aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na aliyekuwa Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Je, mpaka hapo Kikwete, Mangula na
Kinana wanawezaje kuingizwa katika uongo huo kwamba eti walifanikiwa
kuishawishi Kamati Kuu ya CCM kuvunja Katiba na Kanuni zake?
Au, kama ni kweli walifanya hivyo na
Kamati Kuu kuteua majina hayo matano badala ya sita, saba, nane, tisa au zaidi
na kupelekwa NEC kwenda kuchujwa na kubaki matatu yaliyopelekwa kwa Wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa Taifa, kule ambako hatimaye alipatikana mgombea urais huo ni
usaliti au ni kukidhi matakwa ya Katiba?
Nafahamu pia kuwa Kingunge alikuja
na shutuma kuwa Kamati Kuu haikuwaita ili kuwaona, kuwasikiliza ama kuwahoji
wana CCM 38 waliokuwa wakiomba uteuzi wa kugombea urais kwa sababu kubwa moja
tu: kukatwa kwa jina la rafiki yake aliyetaka awe ndiye Rais wa Serikali ya
Awamu ya Tano, Edward Lowassa.
Kama huo ni uongo kama inavyoweza
kudaiwa na baadhi ya wapambe wake mwenyewe, wapambe wa Lowassa na hata
vinginevyo, mbona hakuonyesha ibara ama kifungu cha Katiba au Kanuni za Uongozi
na Maadili za CCM kilichokiukwa?
Jambo la mwisho ninalotaka kulitolea ufafanuzi hapa ni madai kuwa, wana CCM ambao wameadhibiwa "wamehukumiwa kwa usaliti wa kuendana na mchakato wa kumpata mgombea urais" mwaka 2015.
Sitaki kuwataja wale waliovuliwa
uanachama, kusimamishwa uongozi au kuonywa kwa sababu kila mfuatiliaji wa
masuala ya kisiasa anawafahamu, lakini sikubaliani na madai eti kwamba
wameadhibiwa kutokana na kumuunga mkono "mgombea fulani maalum ambaye
ndiye aliyesalitiwa" au kuporwa haki yake!
Swali linalokuja hapa ni je, ni
ibara gani ya Katiba au Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM inayogawa makundi
wagombea urais, kwamba kuna wengine ni maalum na hata vinginevyo?
Ingawa sitaki kusema undani kuhusu
jambo hili, lakini waliovuliwa uanachama ni baadhi ya wasaliti walioihujumu CCM
kutaka ishindwe uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.
Hawakuadhibiwa kutokana na sababu
nyingine yoyote isipokuwa hiyo. Wapo ambao wakati huo walikuwa "wana CCM
mchana", lakini ikifika usiku hubadilika na kuungana na wapinzani kwa
kuwasaidia washinde.
Wapo waliofanya hivyo na kujitanda
kwa baibui kusudi wasifahamike sura zao, na pia kuna wengine waliokuwa
wakivujisha siri zote za mikakati ya CCM kwenda Chadema, Civic United Front
(CUF) au vyama vingine vya upinzani nchini.
Wapo wana CCM waliowapigia kampeni
wapinzani, na pia kuna wengine waliotoa mpaka raslimali fedha, watu au magari
yao na kadhalika ili mradi tu washinde na kukamata madaraka ya dola.
Hapo ndipo nahitimisha kwa kusema
Kingunge asidhani kuwa Kikwete, Mangula au Kinana anaweza 'kuwachafua' kwa
kuwatungia uongo.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
No comments:
Post a Comment
ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇