LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 11, 2012

CHADEMA WAJIPENYEZA MAANDAMANO YA WAANDISHI DAR KUPINGA MAUAJI YA MWANGOSI

Kada wa Chadema, Dk. Lwaitama kwenye maandamano hayo
DAR ES SALAAM, TANZANIA
Maandamano ya Waandishi wa habari kulaani mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten, Daud Mwangosi yameingia doa baada ya waandishi kumfukuza Waziri lakini wakamkaribisha kada wa Chadema kuwahutubia.

Dosari hiyo, ilijitokeza leo, mwishoni mwa maandamano hayo kwenye viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, baada ya waandamaniji kufika wakiwa na viongozi wao wakiwemo kutoka Jukwaa la Wahariri.

Mara msafara huo ulipofika, pembezoni mwa viwanja hivyo, ukakumbana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi alikiwa eneo hilo na mara akaungana na baadhi ya viongozi wa waandishi, ambao walijaribu kutaka kumtamtambulisha.

"Hatuatakiii, aondoke, aondoke!" waandishi wa habari kwenye maandamano hayo walipaza sauti huku wengine wakirusha mikono kuashiria kukataa kabisa waziri Nchini asizungumze lolote au kuwepo kwenye mkutano mwishoni mwa maandamano hayo.

Baadhi ya viongozi wa Jukwaa la Wahariri akiwemo Nevil Meena, walijaribu kuwatuliza waandishi lakini, ikashindikana na kwa busara Waziri Nchini akaamua kuondoka.

Hata hivyo katika kinachoonyesha kwamba kulikuwepo tofauti kati ya waandishi kuhusu kumkataa Dk. Nchimbi, baadhi yao walimfuata na kumhoji, lakini wengine wakaingilia kati kuzuia mahojiano hayo.

"Sasa tumesema aondoke halafu mnamhoji, mnamhoji nini na tumekataa hapa asiseme nini? mwacheni njooni kwenye mkutano wetu hapa, kwanza sijui habari hizo mtazirusha wapi, sisi ndiyo wahariri", zilisikika sauti zikipazwa.

Baada ya kuzungumza viongozi mmoja baada ya mwingine, wote wakilaani kwa nguvu zote mauaji ya Mwangosi, nayoaminika kufanywa na polisi wakati wa maandamano ya Chadema, Septemba 2, mwaka huu, mkoani Iringa, ndipo akapandishwa jukwaani Kada wa Chadema, Dk. Azaveri Lwaitama.

Dk. Lwaitama ambaye amewahi kushiriki shughuli nyingi za Chadema ikiwemo mikutano ya chama hicho, alipandishwa jukwaani mmoja wa viongozi wa Jukwaa la Wahariri.

"Jamani mnajua waandishi wa habari tuna marafiki. Sasa hapa tunaye Dk. Lwaitama amabaye ni rafiki yetu atazungumza machache", alisema Misango akimkaribisha Dk. Lwaitama.

Akizungumza, Lwaitama aliwataka waandishi wa habari kutowachukia polisi wadogo akisema, wao siyo tatizo ila tatizo ni wakubwa zao ambao alidai wanatumwa na wanasiasa kutekeleza matakwa yao.

"Sasa kama Chadema wanafungua matawi ya chama chao, kwa nini utumie polisi kuwazuia? si na wewe ukafungue matawi yako?" alisema Dk. Lwaitama katika moja hoja zake kwenye mkutano huo.

Kufuatia Dk. Lwaitama kuzungumza habari za vyama vya siasa hadi kutaja majina, baadhi ya viongozi na waandishi walianza kulauminiana kuonyesha kwamba walichofanya nin kosa.

"Sisi tulikuwa tumeshakubaliana kwamba asishirikishwe kada wa chama chochote wala wanaharakati, sasa huyu Lwaitama nani amemruhusu kupanda jukwaani?, alihoji mmoja wa viongozi wa Klabu wa Waandishi wa habari wa Dar es Salaam.

Maandamano ya waandishi hao yalianzia kituo cha Channel Ten, jijini, saa tatu asubuhi, na kuendelea hadi kwenye viwanja hivyo vya Jangwani, baada ya kupitia barabara ya Morogoro.

Polisi walisindikiza maandamano hayo baadhi wakiwa nyuma na gari lao na wengine wakitembea kwa miguu, hadi kwenye viwanja hivyo, ambako halimalizika salama.

4 comments:

  1. Dr Azaveri Rwaitama Ni Mwanachama wa CCM aliye Mfu

    ReplyDelete

  2. Kimsingi na kiuzoefu, ni vigumu kuiepuka siasa katika suala hili la mwandishi huyu aliyeuawa.
    Kwa maoni yangu,tukio hili ni miongoni mwa yanayopunguza alama za C.C.M. miongoni mwa wananchi.

    ReplyDelete
  3. Nimesoma habari yenu juu ya Chadema kuvamia maandamano, binafsi napenda kushauri CCM itafute suluhu katika kujibu hoja na matakwa ya wananchi, kwa uelewa wangu ni kwamba vyombo vya habari vina umiliki mpana, kutoka mtu binafsi hadi taasisi, kuna vyombo vya habari vya kichama, nina imani hata siku ya maandamano waandishi wa habari ambao ni wa mlengo wa CCM walikuwepo na walishiriki vema. Tatizo ni pale Mhe, Waziri anapoingilia maandamano bila idhini ya Wahusika, kwani ilikuwa tabu gani waziri kuomba mwaliko ili apokee maandamano yale? Binafsi sioni kama kuna suala la chama fulani, bali naona kukiukwa kwa taratibu za maamdamano, tena na Mhe, Waziri ambaye ana dhamana ya ulunzi wa raia na mali zao. Ni katika mantiki hii nashindwa kumuelewa nchimbi, je kama ingetokea mtu yeyote akapigwa na kitu kizito au kutokea vurugu polisi wangetakiwa kumkamata nani? CCM mjitafakari katika mienendo yenu. Mnapunguza kura kwa matendo yenu

    ReplyDelete
  4. Bwa Godbless, ni kweli CCM lazima ijitafakari, maana hali hii ya Chadema kuona imeshindwa kwa sera na sasa ikaanzisha hii propaganda ya kupanga maandamano ya lazima ili yatokee maafa halafu CCM ndiyo ionekane imeua, kweli inainyima kura CCM.

    Kuhusu kuwepo waandishi wa habari kutoka vyombo vya CCM siyo uongo, LAKINI lazima ujue kwamba walishiriki maandamano hayo kwa nafasi yao ya uandishi wa habari au siyo? Sasa tuambie Dk. Lwaitama alishiriki kama nani zaidi ya kuiwakilisha Chadema ambayo ilikuwa lazima uwakilishi wake uonekane kwa kuwa kulikuwa na mkono wake kwenye maandamano hayo? Maana hata wewe unajua kazi na taaluma ya Dk. Lwaitama, si mwandishi. Na hata uzungumzaji wake pale, ulikuwa ule ule wa Chadema.

    ReplyDelete

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages